0




20150810_182328

RAIA wa Burundi aliyetambulika kwa jina la Buchumi Joel (39), amefariki dunia baada ya kuugua ugonjwa wenye dalili sawa na Ebola, ikiwa ni pamoja na kutokwa na damu sehemu mbalimbali za mwili wake.

Madaktari, wauguzi na ndugu waliomuhudumia mgonjwa huyo, wamewekwa chini ya uangalizi maalumu kwa siku 21 kama hatua ya tahadhari, huku wakisubiri kupokea majibu ya sampuli za vipimo ili kubaini iwapo kweli ni ugonjwa wa Ebola ama la.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, daktari wa Shirika la Kimataifa linaloshughulika na Wahamiaji (IOM), Dk. Laurian Beda, alisema Joel aliingia Kigoma mwaka 2012 na kuishi kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu, Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma kwa muda wa miaka mitatu akiwa pamoja na familia yake.

Alisema akiwa kambini hapo alikuwa akisumbuliwa na maradhi, hivyo Julai 28 mwaka alisafiri hadi Kigoma Mjini pamoja na familia yake kwa ajili ya kusafirishwa na IOM kwenda nchini Marekani.
“Akiwa Kigoma, alifikia katika hosteli za Hoteli ya Nzimano, lakini Julai 31 mwaka huu alianza kuugua akitokwa na damu sehemu mbalimbali za mwili mdomoni, kwenye fizi na machoni, na ilipofika Agosti 8, mwaka huu hali yake ilizidi kuwa mbaya, ndipo uongozi wa shirika uliamua kumpeleka katika Hospitali ya Mkoa wa Kigoma ya Maweni kwa ajili ya matibabu zaidi,” alisema Beda.

Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Maweni, Dk Shija Ganai, alithibitisha kupokewa kwa mgonjwa huyo na kumlaza wodi namba nane, lakini wakati wakiendelea kumtibu, usiku wa kuamkia jana hali yake ilibadilika na kuwa mbaya, na alfajiri alifariki dunia.

“Kutokana na dalili hizo, tunadhani ugonjwa huo unaweza kuwa Ebola, hivyo tumechukua sampuli za vipimo vyake kwa ajili ya kufanya uchunguzi zaidi na kuvipeleka maabara kuu ya Taifa kwa ajili vipimo ili kubaini ugonjwa uliosababisha kifo chake,” alisema.

Dk. Ganai, jana aliliambia Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), kwamba dalili za mgojwa huyo hazithibitishi moja kwa moja kwamba alikuwa akiugua Ebola.

Swali: Kuna taarifa kwamba kuna tukio la mtu kafa kwa Edola, Kigoma, hili lina ukweli kiasi gani?
Jibu: Tukio hili ni la kweli, japokuwa katika viwango vya kuthibitisha ugojwa huo, dalili zake hazitoshi kuthibitisha kwamba alikuwa akiugua Ebola. Kwenye kundi la magonjwa yenye dalili sawa na za Ebola, yapo 18 Ebola ikiwamo, lakini kwa mgonjwa huyu kwa dalili alizozionyesha, haithibitishi kwamba ni mgojwa wa Ebola.

Swali: Huyo mgojwa alikuwa na dalili gani?
Jibu: Alikuwa anatoka damu kwenye mdomo, macho mekundu sana, nesi aliyekuwa akimuhudumia alithibitisha kuwa alikuwa anatokwa damu kwenye macho, alikuwa anahangaika sana, lakini hakuwa na homa kali.

Mtu huyu katoka kambi ya Nyarugusu, lakini siyo miongoni mwa wale wakimbizi wapya. Wakati kambi zinafungwa, wakimbizi wengine walihamishwa na huyu ni mmoja wa wakimbizi aliyetoka kambi ya Mtabila na kuhamishiwa kambi ya Nyarugusu, ana kama miaka mitatu yupo pale kambi ya Nyarugusu.

Kuna dalili ambazo zote zikiwapo, hata kabla ya vipimo vya maabara tunaweza kusema kuwa tunahisi ni Ebola, lakini kwa huyu zile dalili hazithibitishi, pamoja na kwamba tumeshachukua vipimo, lakini dalili zake tayari zinamwondoa mgonjwa huyu kwenye kundi la Ebola, ila ni miongoni mwa magonjwa yanayosababisha mgonjwa kutokwa damu katika baadhi ya maumbile yake.
Swali: Ikiwa ni Ebola, Tanzania imejiandaa vipi kukabiliana na ugonjwa huo?

Jibu: Kama itathibitika, sisi kwa mkoa tuna mpango tuliotengeneza kwa kushirikiana na wizara, katika hiyo tunaandaa vifaa, madawa na sehemu za kutunza wanaopata ugonjwa huo.
Mwili umeshazikwa kwa taratibu na tahadhari zote, ulizikwa na wataalamu wa afya wakiwa wamechukuwa tahadhari za kutosha ili wasipate maambuzi yoyote.

Post a Comment

 
Top