0
 
Marais John Magufuli na Paul Kagame wakiwasha mwenye eneo la Gisozi
Rais wa Tanzania John Magufuli amesema mauaji ya kimbari sawa na yaliyotokea nchini Rwanda hayafai kuruhusiwa kutokea tena.

Akizungumza mara baada ya kutembelea jumba la makumbusho mauaji ya Kimbari ya mwaka 1994, Rais Magufuli amesema amesikitishwa sana na mauaji hayo.

"Haitatokea tena, hatuwezi kubadilisha yaliyopita lakini tunaweza kubadilisha mambo ya sasa na yajayo, mauaji haya hayapaswi kutokea tena," amesema Dkt Magufuli, kwa mujibuwa taarifa kutoka ikulu.
Rwanda imekuwa ikiadhimisha kumbukumbu ya miaka 22 ya tangu kutokea kwa mauaji ya kimbari yaliyosababisha vifo vya watu takribani 800,000.

Rais Magufuli na mwenyeji wake Paul Kagame waliwasha mwenge utakaowaka kwa kipindi cha siku 100 yaliyodumu mauaji ya kimbari ya Rwanda katika eneo la makumbusho hayo Gisozi.

Mkuu wa kitengo cha Rwanda cha kupambana na mauaji ya kimbari Dkt Jean Damascene Bizimana, akihutubu wakati wa maadhimisho mafupi ya kukumbuka mauaji hayo, amezihimiza nchi za Afrika Mashariki kubuni sheria za kufwatilia na kuwadhibiti watu wanaoeneza itikadi za mauaji ya kimbari.
Amesema nchi za Burundi na Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo zilitoa hifadhi na kushirikiana na wapiganaji wa kundi la FDLR wanaotuhumiwa kutekeleza mauaji hayo.

Amesema Rwanda imefurahishwa sana na taifa la Ujerumani kwa kuwakamata na kuwahukumu vinara wa kundi hilo wanaoishi nchini Ujerumani kutokana na mchango wao katika mauaji yanayotekelezwa na kundi hilo nchini Congo.

Viongozi hao wa FDLR ni Ignace Murwanashyaka aliyehukumiwa miaka 13 jela na Straton Musoni aliyehukumiwa miaka 8 jela.

Mwandishi wa BBC aliyeko Rwanda Yves Bucyana anasema kutakuwa na wiki nzima ya maombolezo kukumbuka waliouawa wakati wa mauaji hayo.

Shughuli za michezo na burudani zimepigwa marufuku huku bendera zikipepea nusu mlingoti.
Dkt Magufuli amekuwa kwenye ziara rasmi ya siku mbili nchini Rwanda, ziara yake ya kwanza nje ya nchi tangu kuingia madarakani Novemba mwaka jana.

Ameondoka Kigali na kurejea Dar es Salaam.

Post a Comment

 
Top