Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC imefungua faili maalumu la kufuatilia hali ya kisiasa na kiusalama ya Burundi.
Bi Fatou Bensouda, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa
ya Jinai ICC amenukuliwa na shirika la habari la Ufaransa akisema leo
kuwa, kumefunguliwa faili maalumu la kufuatilia hali ya Burundi ambayo
tangu mwaka jana imekumbwa na machafuko ya kisiasa.Mwendesha Mashtaka Mkuu wa mahakama ya ICC amesema, wamekuwa wakifuatilia kwa karibu matukio ya Burundi tangu mwezi Aprili 2015 na mara kadhaa wamekuwa wakizitaka pande hasimu nchini huyo zijiweke mbali na machafuko.
Fatou Bensouda ameongeza kuwa, mahakama ya ICC imewaonya kwa mara kadhaa baadhi ya watu nchini Burundi kuhusu uwezekano wa kutendeka jinai nchini humo na namna mahakama hiyo inavyofuatilia kwa karibu kila linalojiri huko Burundi.
Burundi ilitumbukia katika machafuko tangu mwezi Aprili 2015 baada ya wapinzani kupinga hatua ya chama tawala cha CNDD-FDD ya kumuidhinisha Rais Pierre Nkurunzinza kugombea tena urais kwa kipindi cha tatu mfululizo.
Taarifa zinasema kuwa, zaidi ya watu 400 wameshauwa na zaidi ya laki mbili na 50 elfu wamelazimika kuwa wakimbizi nje ya Burundi kutokana na machafuko hayo.
Post a Comment