0


JAMAL Malinzi (57), Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kufikishwa mahakamani mchana huu jijini Dar es Salaam, kujibu tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka.


Taarifa kutoka ndani ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru) zinasema, Malinzi anafikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ambako anatarajiwa kukabiliwa na mashitaka kadhaa ya ufujaji wa fedha za shirikisho, rushwa na matumizi mabaya ya madaraka.


Mbali na Malinzi mwingine anayefikishwa mahakamani pamoja naye, ni katibu mkuu wa shirikisho hilo, Selestine Mwesigwa.


“Ndio. Rais wa TFF na katibu mkuu wake, wote wawili tunawashikilia na watafikishwa mahakamani leo kujibu tuhuma zinazowakabili,” ameeleza kiongozi mmoja mwandamizi wa Takukuru ambaye hakupenda kutajwa jina lake gazetini.

Alipoulizwa kipi hasa kilichoisukuma Takukuru kuwakamata na hatimaye kutaka kuwafikisha mahakamani Malinzi na Mwesigwa, kiongozi huyo alisema, “…hayo mengine yatafahamika mahakamani. Mimi siyo msemaji wa Takukuru.”


Amesema, “ulinichoniuliza, ndicho nilichokujibu. Kama kuna una mengine, mtafute mkurugenzi mkuu wa Takukuru, Mlowola (Valentino Longino Mlowola). Yeye ndiye anayeweza kukueleza kwa kirefu ambacho kinawapeleka watuhumiwa mahakamani.”

Huku Malinzi na Mwesigwa wakipelekwa mahakamani, ndani ya TFF mchana huu wa leo –tarehe 29 Juni 2017 – kumepangwa kufanyika usaili kwa wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi.
Miongoni mwa nafasi hizo, ni rais wa shirikisho hilo, makamu wa rais na wajumbe wa kamati tendaji. Malinzi ni miongoni mwa wanachama wa TFF waliomba kugombea urais.

Malinzi amekuwa anatuhumiwa na wanachama wenzake wa shirikisho hilo kuendesha shirika hilo la umma kama kampuni yake binafsi. Anadaiwa kutenda upendeleo katika kutoa nafasi za uongozi; na au ajira kwa watu wanaotoka katika mkoa wake wa Kagera.

Miongoni mwa wanaotajwa, ni pamoja na katibu mkuu Mwesigwa; Evodius Mtawala, aliyekuwa mkurugenzi wa vyama wanachama na masuala ya kisheria wa TFF na “wakili msomi” – Julius Lugaziya, mwenyekiti wa Kamati ya Rufaa ya uchaguzi ya shirikisho hilo.

Post a Comment

 
Top