0



Habari/Picha Na Jonas Kamaleki
Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu,Bunge, Kazi, Ajira na Watu Wenye Ulemavu itahamia Dodoma juma lijalo kufuatia agizo la Mhe. Rais John Pombe Magufuli la Serikali kuhamia Dodoma.

Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu, Bunge, Kazi ,Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu, Jenista Mhagama wakati akiongea na watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zilizoko chini ya ofisi hiyo.

“Mchakato wa kuhamia Dodoma umekwisha kilichobaki kwa sasa ni utekelezaji, mimi na manaibu mawaziri wangu tunahamia juma lijalo ili tukamkaribishe Mhe. Waziri Mkuu anayehamia Septemba mwaka huu,”alisema Mhagama.

Mhagama amesema kuwa kila kiongozi anayehamia Dodoma inabidi awakute walio chini yake tayari wamekwishahamia ili kumpokea, hivyo akawataka na watendaji ambao wako chini yake watangulie kwa ajili ya kumpokea yeye na viongozi wenzake.

Aidha, Waziri huyo amesema kwa sasa hakuna mjadala wa kuhamia Dodoma lilobaki ni utekelezaji  tu wa kuhamia Makao Makuu.

Mhagama amesema kama kuna Taasisi chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu imetenga fedha kwenye bajeti kwa ajili ya ujenzi, shughuli hiyo ikafanyike Dodoma ambako Serikali inahamia. Kwa kusema hivyo kadhalika na ofisi au Wizara nyingine za serikali ambazo zimetenga fedha ya ujenzi wakajenge Dodoma.

Suala la kuhamia Dodoma sio geni bali limekewepo kwa kipindi kirefu ila utekelzaji wake ndio ulikuwa bado; pia katika Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 suala hili lipo, alisema Mhagama na kuongeza kuwa kipindi cha nyuma Wizara saba (7) ziliwahi kuhamia Dodoma na kwa sasa Wizara inayoshughulikia Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) iko Dodoma.

Waziri Mhagama ameipongeza Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kuanza ujenzi wa jengo lake mjini Dodoma na kusisitiza kuwa Wizara na Taasisi nyingine za Serikali kuiga mfano huo kwa kujenga ofisi zao Dodoma.

“Kwa kuwa sisi ni waratibu wa wizara zote inabidi tuunde kikosi kazi kitakachofanya kazi ya uratibu wa kuhama kikiwa Dodoma ili kuwawezesha na watumishi wenzetu kutekeleza agizo la Mhe. Rais la serikali nzima kuhamia huko,”alisema Mhagama.

Mhagama amesema kuwa Mamlaka ya Ustawishaji wa Makao Makuu Dodoma (CDA) wameshafanya kazi nzuri ya upimaji eneo la serikali ambalo litatumika kwa ajili ya ofisi.
 
“Tumefika mwisho wa mchakato sasa ni utekelezaji na tunataka watumishi walielewe vizuri suala hili na wawe tayari kulipokea,”alisisitiza Mhagama.

Kuhamia Dodoma katika kipindi hiki kunatokana na agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli alillolitoa tarehe 25 Julai, 2016 mjini Dodoma kwenye Mkutano Mkuu Maalum wa CCM ambao ulimchagua kuwa Mwenyekiti wa tano wa chama hicho tawala.

Post a Comment

 
Top