0


Wakati CCM ikijiandaa kumkabidhi Rais John Magufuli uenyekiti, suala la masalia ya Edward Lowassa linaweza kuchukua nafasi kubwa katika vikao vitatu vya juu vinavyofanyika kwa mara ya kwanza tangu kumalizika Uchaguzi Mkuu mwaka jana. 

Ni dhahiri kuwa Mkutano Mkuu Maalumu ulio na ajenda moja tu ya kumchagua mwenyekiti mpya hautakuwa na nafasi ya kujadili ajenda nyingine, lakini Halmashauri Kuu iliyogawanyika baada ya Lowassa kuenguliwa kwenye mbio za urais, inaweza kuchukua muda kujadili CCM mpya baada ya waziri huyo mkuu wa zamani kujiondoa Julai 28 mwaka jana.

CCM itaanzia mikutano yake kwa kikao cha Kamati Kuu, ambayo hufanya maandalizi ya kikao cha Halmashauri Kuu kitakachofanyika Ijumaa na kumalizia na Mkutano Mkuu Jumamosi wiki hii.

Pia kutakuwa na kikao kingine cha Halmashauri Kuu kitakachofanyika Jumapili ambacho kwa sehemu kubwa kinatarajiwa kujadili taarifa za wasaliti zilizoandaliwa na kamati za siasa za mikoa na huenda kikatoa maamuzi mazito yanayobeba mustakbali wa kuijenga “CCM ya Magufuli”.

Lakini makada wengi waliohojiwa  kuhusu suala la masalia ya Lowassa kuibuka kwenye vikao hivyo, walipinga wakisema waliomuunga mkono mwanasiasa huyo maarufu, walifanya hivyo wakati akiwa CCM na kwa kuwa hawakumfuata hawatarajii suala hilo kuibuka tena.

“Makundi ndani ya CCM yalikwisha baada ya Magufuli kupitishwa kukabidhiwa kijiti,” alisema mwenyekiti wa CCM wa mkoa wa Geita na mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Kasheku Msukuma alipoulizwa kuhusu suala la Lowassa kuibuka kwenye vikao hivyo vya juu.

Msukuma, ambaye alifanya mbwembwe za kuhama kambi ya Bernard Membe kwa kutua na helikopta kwenye mkutano wa Lowassa mjini Arusha, alisema wakati CCM ikisaka mgombea wake wa urais, kulikuwa na makundi zaidi ya 40.

“Wakati ule kila mgombea alikuwa na kundi. Ila kwa sasa sidhani kama hali hiyo bado ipo maana baada ya mgombea kupatikana kila mmoja alimuunga mkono,” alisema Msukuma.

Kauli kama hiyo ilitolewa na mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhan Madabida ambaye alisema kila mwenyekiti huja na timu yake, hivyo kama kutakuwa na mageuzi, si kitu kinachohitaji mjadala. 

“(Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin) Mkapa alipomuachia uenyekiti (Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya) Kikwete alikuja na timu yake mpya. Kama utakumbuka katibu mkuu wake alikuwa Yusuf Makamba,” alisema Madabida ambaye naye alikuwa miongoni mwa wenyeviti waliomuunga mkono Lowassa.

“Nina matarajio na rais. Naamini atakifanya chama kuwa imara zaidi na kuleta mageuzi ya kisiasa na kiuchumi. Mabadiliko ni kawaida na wenyeviti wapya huja na kamati kuu na sekretarieti mpya.”

Hata hivyo, kuanzia Januari mwaka huu kamati za siasa za mikoa zimekuwa zikikutana kujadili watu wanaoitwa ni wasaliti na kupeleka mapendekezo ya hatua dhidi yao kwenye vikao vya juu.

Rais Magufuli, ambaye hajawahi kushika uongozi wa chama, anaaminika kuwa ataifanya CCM kuwa na sura, mwelekeo na ushawishi mpya, hali itakayochangia kukata mizizi iliyojengwa na wanasiasa mashuhuri.

Kutokana na hali ilivyokuwa wakati Lowassa akiondoka CCM na mtikisiko aliouacha, chama hicho hakitaweza kujipapatua bila kumtaja Lowassa na mtandao wake wakati kikijadili jinsi ya kusonga mbele.

Mbunge huyo wa zamani wa Monduli amekuwa akijadiliwa kwa ushabiki mkubwa ndani na nje ya vikao halali vya CCM tangu alipojitokeza kwa mara ya kwanza mwaka 1995 kuwania urais akiwa na umri wa miaka 42.

Kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2015, mwanasiasa huyo aliwagawa makada wa CCM na alipohamia Chadema kuna kundi lilimfuata na jingine kubakia, huku baadhi ya wanachama kwenye kundi hilo wakituhumiwa kwa usaliti.

Baada ya kujiondoa CCM Julai 28, 2015 na kujiunga Chadema alikoteuliwa kuwa mgombea urais na kuungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), mashambulizi mengi kutoka CCM yalielekezwa kwake.
 
Vikao vinavyosubiriwa kutia muhuri mapendekezo ya kamati za siasa za mikoa ndivyo vinavyofanyika wiki hii mjini Dodoma baada ya CCM kuitisha mkutano mkuu maalumu ili kukamilisha taratibu za kumkabidhi Rais Magufuli usukani wa chama hicho.

 Halmashauri Kuu ya JPM 
Halmashauri Kuu ya JPM inatarajiwa kutumbua watendaji wazembe, goigoi, wasiokwenda na kasi yake, wabadhirifu wa fedha za chama na wengine ambao uwapo wao ni mzigo kwa CCM.

Hivyo, Halmashauri Kuu itasuka upya chama, pia kwa kujaza nafasi za watendaji waliojiuzulu kutokana na desturi ya chama hicho.

Kwa kawaida, CCM inapopata mwenyekiti mpya, sekretarieti yote hujiuzulu ili kumpa nafasi kiongozi huyo kupanga safu yake, alisema msemaji wa chama hicho, Christopher Ole Sendeka juzi alipoongea na waandishi wa habari mjini Dodoma.

Sekretarieti inaongozwa na katibu mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, ambaye anaaminika kuwa alifanya kazi kubwa ya kukirudishia chama hicho nguvu wakati wa kuelekea Uchaguzi Mkuu uliopita ambao ulikuwa na ushindani mkubwa.

Wengine ni Vuai Ali Vuai (Naibu Katibu Mkuu Zanzibar), Rajab Luhavi (Naibu Katibu Mkuu Bara), Mohamed Seif Khatib (Katibu wa Oganaizesheni) na Nape Nnauye (Katibu wa Itikadi na Uenezi).

Wengine ni Dk Asha-Rose Migiro (Katibu wa Idara ya Mambo ya Nje), na Zakia Meghji (Katibu wa Uchumi na Fedha).

Halmashauri Kuu ya JPM inatarajiwa pia kujadili hali ya hewa ya kisiasa ndani ya chama, kupanga mikakati ya kuimarisha uchumi na kutekeleza mapendekezo ya kuwafukuza wasaliti, ambao wanatuhumiwa kuwa waliendelea kumuunga mkono Lowassa wakati wa kampeni na kusababisha chama kupoteza baadhi ya majimbo.

 Oktoba 30, 2015 baada ya kukabidhiwa cheti cha ushindi wa urais na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damian Lubuva iliandaliwa hafla fupi makao makuu ya CCM Lumumba, ambako Dk Magufuli alimwambia mwenyekiti wake akisema: “Umezungukwa na wanafiki na watu ambao ulidhani watakusaidia kwenye chama, lakini wamekuangusha”  

Miongoni mwa watu ambao hata wakati wa kampeni alikuwa anawashutumu ni waliowahi kushika nyadhifa za juu serikalini, lakini wakahamia upinzani na kuibeza Serikali.

 Dk Magufuli anaonekana alikuwa anawalenga Lowassa na mwenzake Frederick Sumaye ambao waliunda safu kabambe ndani ya Chadema kuisakama CCM.

Orodha ya watakaotumbuliwa na NEC ya JPM ni ndefu. Baadhi yao ni makada waliojitokeza hadharani kupinga utaratibu uliotumiwa na wazee kukata jina la Lowassa kugombea urais. 

Hata baada ya CCM kumteua Dk Magufuli kuwa mgombea urais, bado wapo waliompinga wakidai hana mizizi katika chama.

Wengine wanaoweza kutumbuliwa ni walioanzisha wimbo wa “Tuna imani na Lowassa” ndani ya kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM wakionyesha utiifu wao kwa Lowassa badala ya Mwenyekiti Kikwete aliyeongoza kikao cha Kamati Kuu kilichotoa majina matano ya waliopitishwa kugombea urais bila ya jina la Lowassa kuwamo.

Wengine wanaoweza kutupiwa virago ni makada waliosusa kumpigia debe Dk Magufuli pamoja na waliodaiwa kukitelekeza chama.

Habari nyingine zinasema waliopendekezwa kufukuzwa na vikao vya wilayani ni wanaodaiwa kubadilika usiku na kusaidia Ukawa, wakiwamo wenyeviti wa mikoa na makatibu.

Pia, wamo baadhi ya wabunge na wafanyabiashara waliokuwa wanawabeba mamia kwa makumi ya wanachama kwenda nyumbani kwa Lowassa mjini Dodoma kuonyesha kumuunga mkono

Post a Comment

 
Top