UCHUMI
wa Tanzania unazidi kukua kwa kiwango cha asilimia 7 kwa mwaka kutokana
na juhudi za makusudi zilizofanywa na Serikali ikiwemo kuimarisha
miundombinu, ukuzaji wa teknolojia ya habari na mawasiliano na uchimbaji
wa madini.
Hayo
yamesemwa leo mjini Dodoma na Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa
Majaliwa wakati alipokuwa akizindua Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa
Miaka Mitano 2016/2017- 2020/2021.
Majaliwa
alisema Mpango huo unalenga kuboresha maisha ya Watanzania kijamii na
kiuchumi ili kuwaondolea umaskini kwa kuweza mkazo katika sekta za
kilimo, mifugo, uvuvi na viwanda.
“Umaskini umepungua kwa asilimia 6.2 na bado tunaendelea kufanya juhudi kubwa ili kupunguza umaskini,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa na kuongeza kuwa watanzania 10.78 milioni bado ni maskini.
Kwa
mujibu wa Majaliwa alisema kuwa ukuaji wa uchumi inabidi uwe shirikishi
kwa kila mwananchi kushiriki katika shughuli za uzalishaji mali.
Akizungumzia
suala la uwekezaji katika viwanda, Majaliwa alisema Watanzania
wanapaswa kuwezeshwa katika kupata mitaji ya kuwekeza na kuifanya
Tanzania kuwa nchi ya viwanda na kufikia uchumi wa kati.
Kwa
upande wake Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango alisema
wakati umefika wa kuhakikisha ukuaji wa uchumi unatiliwa mkazo na
serikali kwa kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji hasa katika viwanda na
madini.
“Tumeamua
kuboresha miundombinu ikiwemo ya ujenzi wa reli, kuboresha bandari zetu
na kufufua Shirika la Ndege (ATCL) na kutekeleza miradi mikubwa ya
uchimbaji wa makaa ya mawe ya Mchuchuma na Liganga ambavyo vitaongeza
pato la mtanzania kutoka dola za Kimarekani 1006 hadi 1500 ifikapo
2020,” amesema Dkt. Mpango.
Mpango
huu wa Maendeleo ambao umezinduliwa na Mhe. Waziri Mkuu una Kauli Mbiu
isemayo “Kujenga Uchumi wa Viwanda ili kuchochea Mageuzi ya Uchumi na
Maendeleo ya Watu”.
Post a Comment