0

wanawake wa Ukawa wakitoka nje 1
*Wabunge viti maalumu Ukawa wadai kudhalilishwa, watolewa kwa nguvu na askari ndani ya ukumbi
Na Bakari Kimwanga, Dodoma

BUNGE limechafuka, ndivyo unavyoweza kusema baada ya Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Akson, kushindwa kutuliza hasira za wabunge wanawake wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na hivyo kuwaamuru askari wa Bunge kuwatoa nje ya ukumbi wa Bunge.

Hasira za wabunge hao zilitokana na kile walichokiita majibu yasiyo ya kuridhisha na ya upendeleo ya Naibu Spika huyo katika kushughulikia hoja waliyodai imewadhalilisha iliyotolewa na Mbunge wa Ulanga Mashariki, Goodluck Mlinga (CCM).

Juzi wakati akichangia, Mlinga alisema ili mtu aingie Chadema na awe mbunge wa viti maalumu lazima aitwe ‘baby’. Neno ambalo lilionekana kuwakasirisha wabunge hao wanawake.
Kwa mujibu wa Kamusi ya Oxford toleo la saba, tafsiri ya neno ‘baby’ ni neno linalotumika kumuita mwanamke mdogo, mke wako, mume au mpenzi.

Zaidi kamusi hiyo inaeleza kama neno hilo litatumika kumuita mwanaume au mwanamke ambaye huna uhusiano naye na humfahamu utaonekana umemshambulia na kumuumiza.

Hatua iliyofikiwa jana ya wabunge hao hadi kutolewa nje ya ukumbi wa Bunge ilikuja baada ya kudai kutoridhishwa na majibu ya Naibu Spika huyo waliyoyaita kuwa ni ya upendeleo na kukataa kujibu mwongozo ulioombwa na Mbunge wa Viti Maalumu, Sophia Mwakagenda (Chadema).

Mwakagenda katika mwongozo wake alikiambia kiti cha Spika kuwa anapinga dhana ya wanawake ndani ya Chadema kupata uongozi kwa njia ya uzinifu kama ilivyodaiwa na Mbunge huyo wa Ulanga, Mlinga juzi jioni wakati akichangia bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria.

Hata hivyo, majibu ya Naibu Spika huyo kwamba suala hilo alikwishalitolea ufafanuzi juzi na kutoa maelekezo ya kufutwa kwa maneno yale kwenye taarifa rasmi ya Bunge kwa kuwa pande zote mbili zilitumia maneno ya kuchukiza, yalionekana kuwakera wabunge hao ambao walitaka kuona kiti cha Spika kikitoa adhabu kwa mbunge huyo wa Ulanga.

Hali hiyo ilizua mtafaruku ndani ya Bunge na hata kusababisha wabunge hao kutupa vitabu vya hotuba ya bajeti ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji huku kelele za kuitana ‘baby’ zikishamiri ndani ya Ukumbi wa Bunge.

HALI ILIVYOANZA
Baada ya kipindi cha maswali na majibu saa 4:21 asubuhi Mbunge huyo wa Viti Maalumu, Mwakagenda (Chadema), alisimama na kuomba mwongozo kwa kutumia kanuni ya 68 (7) kuhusu jambo lililotokea ndani ya Bunge.

“Mheshimiwa Naibu Spika nasimama kwa kifungu cha 68 (7). Serikali imeridhia mikataba mbalimbali ukiwemo wa Maputo Protocol (Itifaki ya Maputo) juu ya haki ya mwanamke kuingia kwenye nafasi mbalimbali za uongozi.

“Jana (juzi) wakati mheshimiwa akichangia kwa Wizara ya Katiba na Sheria, alisema wanawake wa upande wa Chadema tumeingia bungeni kwa sababu ya kuitwa ‘ma-baby’.

“Mheshimiwa Naibu Spika, Rais wetu amefanya vizuri sana kutimiza ahadi hii hata wewe amekuteua kuwa mbunge na ukachaguliwa kuwa Naibu Spika kwa sababu ya Maputo Protocol.
“Sitaki kuamini kama wanawake wote humu ndani wamepitia mchakato wa uzinifu ili wapate uongozi. Mimi kama mama kama mwanaharakati, mfumo dume uliojikita kwa wananchi na wanasiasa kwamba kila mwanamke ni mzinzi naupinga na ninataka unipe mwongozo je, hii ni sahihi?” alihoji Mwakagenda.
Wakati wote mbunge huyo akiwasilisha hoja yake hiyo hali ya ukumbi ilikuwa tulivu na kila mbunge akimsikiliza kwa makini.
Pamoja na hali hiyo, mbunge huyo alisema kauli za udhalilishaji dhidi ya wanawake wabunge zilizotolewa na mbunge huyo wa CCM, hazikupaswa kushangiliwa na wabunge wote hasa wanawake.
“Lakini humu ndani tuna vyama vyetu vya kibunge kikiwemo kile cha TWPG (Chama cha Wabunge Wanawake Tanzania), leo hii (jana) mimi kama mwanachama wa chama hicho natangaza kujivua kwa sababu lengo la chama kile ndani ya Bunge ni kutetea haki za wanawake wanaponyanyaswa.

“Ninaona huzuni mwenyekiti pamoja na wadau wengine wa chama hicho wanashangilia udhalilishwaji usiokuwa na vidhibiti.

“Ninaomba mwongozo wako juu ya suala hili na huko nje wanaofikiri kila mwanamke ni mzinifu,” alisema mbunge huyo katika mwongozo wake.

Baada ya kuhitimisha hoja yake mbunge huyo, wabunge wote wanawake wa Ukawa walisimama tena kuomba mwongozo jambo lililopingwa na Naibu Spika ambaye naye alisimama akiwasihi wabunge hao kuketi.
Dk. Tulia alitumia dakika 1:07 kuwatuliza wabunge wa upande wa Ukawa waliokuwa wamesimama wakiomba mwongozo huku nao wakirusha vijembe kwa kumwita Naibu Spika huyo ‘baby’.

“Esther Bulaya tafadhali, Esther Bulaya tafadhali, waheshimiwa wabunge naomba mkae, naomba mkae (walipoketi wote akaendelea), natumia kanuni ya 68 (7).

“Jana (juzi) nilisimama hapa, niliposimama sasa hivi baada ya yale maneno ambayo niliyatolea ufafanuzi kwa maana ya kwamba pande zote mbili zilizopo humu bungeni zilitumia maneno mabaya na nilitoa maelezo kwamba maneno yale yafutwe kwenye taarifa rasmi ya Bunge na tukaendelea tukapitisha bajeti,” alisema.

Kabla hajamaliza maneno hayo wabunge wa Ukawa walisimama tena wakiomba mwongozo huku wengine wakinyoosha karatasi juu ili waonekane.

Kutokana na hali hiyo, Naibu Spika huyo alisema: “Waheshimiwa mliosimama naomba mkae, naomba mkae mliosimama naomba make, waheshimiwa mliosimama naomba mkae.”

Wabunge hao waliendelea kuomba miongozo na wabunge wanawake wengi wakasimama wakilazimisha kupewa mwongozo huku wengine wakiwasha vinasa sauti vyao wakimuita Dk. Tulia ni mkuu wa ‘ma-baby’.

Wakati tafrani hiyo ikiendelea, askari wa Bunge walilazimika kuwaondoa wageni wa wabunge waliokuwepo kwenye ukumbi wa Spika wakifuatilia shughuli za Bunge.

Wakati wageni hao wakiondolewa, askari wengine wa Bunge waliingia ndani ya ukumbi kuwatoa wabunge wanawake wa Ukawa ambao walikuwa wakivitupa vitabu vya hotuba ya bajeti ya matumizi kwa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.

NJE YA UKUMBI
Wakiwa wamezungukwa na askari nje ya ukumbi wa Bunge, wabunge hao wanawake wa Ukawa walitangaza kujitoa rasmi kwenye Chama cha Wabunge Wanawake (TWPG) kwa madai ya kudhalilishwa.
Hatua hiyo ilionekana kumvuruga Mwenyekiti wa TPWG ambaye pia ni Mbunge wa Urambo Mashariki,  Margareth Sitta (CCM).
Sitta alitumia muda mwingi nje ya ukumbi wa Bunge akiwaomba wabunge wa Ukawa wasijitoe kwenye chama hicho.
Alisema anaweza kuzungumzia suala hilo vizuri endapo Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho, Suzan Lyimo (Chadema), ataungana naye kuwasihi wabunge hao wasijitoe kwenye TPWG.

ULINZI WAIMARISHWA
Gazeti hili lilishuhudia askari wa Bunge wakiwa wamezingira Ofisi za Kambi ya Upinzani Bungeni wakati wabunge hao wanawake wakifanya kikao chao cha ndani baada ya kutolewa ndani ya ukumbi wa Bunge kwa amri ya Naibu Spika.
KAULI ZAO
Akizungumzia suala hilo kwa niaba ya wabunge wenzake wa Ukawa, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema), alisema Naibu Spika amevunja Katiba kwa kukataa kuwaruhusu kutoa miongozo yao kwa mujibu wa kanuni za Bunge.

“Tumefanya kikao chetu na tumemaliza hapa na sasa tunaendelea lakini kwa hatua za awali tunatangaza kujitoa katika TPWG, suala hili litakwenda sambamba na kuwaandikia barua wahisani wa chama hiki kuwaeleza kwa kina hatua ya kujitoa kwetu.

“Haiwezekani Katiba inavunjwa Naibu Spika amechagua upande halafu bado tubaki tukiendelea kuangalia tu, sasa kwa hili hapana maana na yeye ni mbunge wa kuteuliwa, je, tuamini naye amepitia mchakato huo wa udhalilishaji. Jibu ni hapana, hatuwezi kuendelea kukaa kimya kwa ajili ya kusikiliza na kuona udhalilishaji kwa wanawake.

“Wanaogopa siku hizi ndio maana wanajificha, wanajua kuwa wakiwa ‘live’ tutafichua uovu na ufisadi wao, hivyo juzi walikuwa na kikao chao cha chama…

“Nadhani hayo ndiyo waliyokubaliana huko ili wajifiche na kuanza kututukana, hatuwezi kukubali kudhalilishwa na upuuzi huu uendelee, hatutaki matusi,” alisisitiza Mdee.

Alisema wataangalia namna ya kuanzisha chama cha wanawake cha wabunge kama Ukawa na watapeleka hoja hiyo kwa Spika na viongozi wote wa Bunge kwa kuwa chama kilichopo hakina msaada kwao.
Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), alisema maneno yaliyotolewa dhidi ya wabunge wanawake wa Ukawa ni ya kipuuzi na si ya kibunge na sehemu yaliyotolewa si mahala pake.
Alisema wakati maneno hayo yakitolewa mjadala uliokuwa unaendelea ulikuwa ni Katiba na Sheria, lakini kwa sababu CCM walikasirishwa na maoni ya Kambi ya Upinzani ndio maana walitoa maneno hayo.
VIJEMBE NDANI YA BUNGE
Wakati wabunge wanawake wa Ukawa wakitoka nje, baadhi ya wabunge wa CCM waliwasha vinasa sauti vyao wakisema: “Halima Mdee arudi ndani mwenzetu.”

Mbunge wa Simanjiro, James Ole- Millya (Chadema), aliwasha kinasa sauti akamuuliza Naibu Spika: “Na wewe ni baby wa Magufuli?”

Vijembe na maneno ya kuudhi viliendelea ndani ya ukumbi wa Bunge ndipo Naibu Spika alipowatuliza kwa muda na kuruhusu mjadala kuendelea.

Baada ya vurugu kutulia, Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema) na Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche (Chadema), walisimama kuomba mwongozo lakini Naibu Spika huyo aliwakatalia.

Baada ya ombi lao kukataliwa Msigwa alisema: “Acha kutuburuza bwana,” huku akiwa amekasirika na kuchukua vifaa vyake na kutoka nje.

Heche akiwa amesimama alisema: “Sisi si wanafunzi wala wewe si ‘headmaster’ (Mkuu wa shule) usituburuze kwanini unatunyima kuongea? Unakiuka kanuni.”

Hata hivyo, Naibu Spika alimwamuru Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, aendelee kuwasilisha hoja yake mbele ya wabunge wengi wa CCM waliobaki ndani ya ukumbi huo.

Post a Comment

 
Top