Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Marekani linaloshughulikia masuala ya kijeshi
barani Afrika, Meja Jenerali Darrly Williams, amemtunuku mkuu wa majeshi
ya vikosi vya nchi kavu Tanzania Meja Jenerali James Mwakibolwa nishani
ya ulipuaji bora wa mizinga nchini.
Nishani hiyo ambayo imekuwa
ikitolewa na Rais wa Marekani, alitunukiwa Meja Jenerali Mwakibolwa
baada ya kuwa mstari wa mbele kurudisha amani kwenye nchi zinazokabiliwa
na vita barani Afrika.
Akizungumza wakati wa kufunga mkutano wa
wakuu makamandi wa vikosi vya nchi kavu barani Afrika, uliofanyika
mkoani Arusha, Jenerali Williams alisema jeshi la Marekani barani Afrika,
linamtambua Mwakibolwa kuwa mchapa kazi bora.
“Mwakibolwa ni mtaalamu
sana kwenye masuala ya mizinga, hata tulipokwenda kwenye mafunzo ya
kijeshi katika kambi ya Monduli, tumeona umahiri wake na tuzo hii
anastahili kwa kuwa anafanya vizuri.
“Jeshi la Tanzania limekuwa mstari
wa mbele kutoa kikundi cha M23 kwenye nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Congo (DRC) na yote hayo ni kutokana na uchapakazi wa Jenerali
Mwakibolwa,” alisema Jenerali Williams.
Akitoa maoni yake kuhusu
tuzo hiyo, Jenerali Mwakibolwa aliahidi kuhakikisha Jeshi la Tanzania
linakuwa imara zadi barani Afrika.
Alisema Tanzania inazingatia masuala ya kijinsia katika jeshi hilo na sasa asilimia 25 ya wanajeshi ni wanawake.
“Jeshi
la Tanzania tuna wanawake wenye vyeo vikubwa na wako ambao tumewapa
kazi kwenye idara mbalimbali. Tunaamini mwanamke anaweza,” alisema
Jenerali Mwakibolwa.
Kuhusu maazimio ya mkutano huo, alisema
wanaangalia namna ya kutoa mafunzo ya kupambana na ugaidi wa baadhi ya
wanajeshi wa Afrika.
Naibu Katibu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi
la Tanzania, Immaculate Ngwale alisema mkutano huo umekuwa na faida kwa
kuwajengea uimara askari wake.
Post a Comment