0


Kwa mara nyingine jana wakazi wa Jiji la Tanga walikumbwa na taharuki baada ya kijana mmoja kurusha bomu la mkono chini ya daraja wakati wananchi walipokuwa wakimfukuza baada ya kukurupushwa na polisi.

Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Leonard Paulo alisema kijana huyo alikurupushwa na askari waliokuwa kwenye msako wa kuwatafuta majambazi waliofanya mauaji Aprili 20, mwaka huu katika duka la Central Bakery.

Alisema tukio hilo lilitokea juzi saa mbili usiku kwenye Mtaa wa Makora, Tarafa ya Ngamiani.

Awali, Kamanda Paulo alisema kijana huyo anayekadiriwa kuwa na miaka kati ya 25 na 30, alipokurupushwa alianza kutimua mbio. 
“Alipoanza kukimbia ndipo wananchi wakaingilia kati, walimfukuza na kumshambulia kwa mawe huku wakimpiga na kitu chenye ncha kali kisogoni, ndipo wakati akipelekwa Hospitali ya Mkoa wa Tanga ya Bombo akafariki dunia njiani,” alisema Kamanda Paulo.

Mapema kabla hajafariki dunia, kamanda alisema kijana huyo alipokurupushwa alikimbia akiwa ameshikilia bomu mkononi.

Kamanda aliwataka wakazi wa Tanga kuwa watulivu kwa sababu vyombo vya dola viko katika operesheni maalumu ya kuwasaka walioshiriki mauaji ya hivi karibuni katika hilo la mikate.

Walioshuhuda tukio hilo walisema kijana huyo alishambuliwa na wananchi baada ya kukwapua simu ya mwanamke mmoja katika Mtaa wa Makorora.

Walisema alianza kukimbia na alipoona wananchi wanamfukuza aliwatahadharisha kuwa wakimsogelea atarusha bomu alilokuwa amelishika mkononi.

Kufuatia kutishiwa na bomu hilo, wananchi waliokuwa wakimkimbiza walipiga simu Kituo Kikuu cha Polisi cha Chumbageni kwa ajili ya kupatiwa msaada.

“Kwa hili tunawapongeza polisi. Walitumia dakika chache kufika eneo la tukio lakini walipobaini kwamba ni bomu, wakaamua kuwasiliana na maofisa wataalamu wa kutegua mabomu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi (JWTZ) ambao waliwasili eneo la tukio,” alisema Rajabu Hamis.

Wakizungumza kuhusu tukio hilo, baadhi ya wakazi wa Tanga waliomba vyombo vya ulinzi na usalama kuimarisha ulinzi kwa sababu wamejawa na hofu, kwa kuwa matukio yanayohatarisha amani yanazidi kutokea.

“Hii ni changamoto kwa vyombo vya ulinzi na usalama, matukio haya yanazidi kuwapa hofu wananchi. Mwezi uliopita yalifanyika mauaji makubwa Central Bakery, leo bomu tena,” alisema Kassim Mbughuni.

Post a Comment

 
Top