0



kassimWAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, leo anatarajiwa kuwaongoza Watanzania  katika mazishi ya aliyekuwa Askofu wa kwanza  wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dodoma, marehemu Matias Isuja.

Marehemu Isuja alifariki dunia Aprili 13 mwaka huu katika Hospitali ya St. Gasper ya Itigi mkoani Singida alipokuwa amelazwa akisumbuliwa na saratani ya utumbo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Mazishi,  Peter Mavunde alisema mazishi hayo yatafanyika katika Kanisa Kuu la Paulo Msalaba mkoani hapa.

Alisema Waziri Mkuu anatarajiwa  kuwasili katika Kanisa Kuu la Jimbo la Mtakatifu Paulo wa Msalaba, kuanzia saa 4:30 asubuhi.

Mavunde alisema ibada ya mazishi inatarajiwa kuanza saa 4:30 za asubuhi na itaongozwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Dodoma, Mhashamu Beatus Kinyaiya akisaidiana na Mwenyekiti wa Baraza la Maskofu Tanzania (TEC) Mhashamu Tarcius Ngalalekumtwa pamoja na maaskofu wengine.

Pia alisema Rais Mstaafu wa Awamu ya tatu, Benjamin Mkapa  ni miongoni mwa wageni wanaotarajiwa kuhudhuria mazishi hayo.

‘’Kesho (leo) kuanzia asubuhi saa 2:00 waamini na waombolezaji mbalimbali wataanza kuwasili  kanisani hapo na ibada maalumu ya maziko itaanza,’’ alisema.

Mazishi hayo yanatarajiwa kuhudhuriwa pia na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana, mawaziri, wabunge na watu mbalimbali.

Marehemu Isuja alizaliwa Agosti 14, 1929, katika Kijiji cha Haubi Wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma.
Alianza masomo  yake ya Kikasisi Desemba 24, 1960 akapewa daraja takatifu la upadre kwa ajili ya Jimbo Katoliki la Dodoma.

Juni 26, 1972 aliteuliwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Dodoma na kuwekwa wakfu Septemba 17, 1972 na Januari 15, 2005 aling’atuka kutoka madarakani.

Post a Comment

 
Top