0

 
                         Watatu hao wamewekwa rumande hadi Ijumaa wiki ijayo
Maafisa watatu wamefikishwa kortini Dar es Salaam leo wakishtakiwa kuhusiana na kashfa ya udanganyifu wa riba ya mkopo wa Dola za Kimarekani milioni 600 ambazo zilikopwa serikali ya Tanzania kutoka kwa benki ya Standard ya Uingereza.

Walioshtakiwa ni aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato nchini Tanzania na Mwenyekiti wa ‘Enterprise Growth Market Advisors Ltd’ (EGMA), Bw Harry Kitilya, aliyekuwa Mkuu wa Idara ya Ushirikiano na Uwekezaji wa Benki ya Stanbic Tanzania, Shose Sinare pamoja na aliyekuwa Mwanasheria wa Benki ya Stanbic Tanzania, Bw Sioi Graham Solomon.

Pamoja na makosa mengine, washtakiwa wote wameshtakiwa kwa makosa ya kula njama na kujipatia fedha kwa udanganyifu, kughushi nyaraka na utakatishaji wa fedha haramu kinyume na sheria.

Wote wamekana mashtaka hayo.

Washtakiwa wote watatu wamepelekwa rumande baada ya kukosa dhamana na kesi hii itatajwa tena tarehe 8 Aprili 2016.

Kashfa hii ilitokana na kitendo cha Benki ya Standard kukubali kuipokesha Serikali ya Tanzania kiasi cha Dola milioni 600 mwaka 2012 kwa masharti ya kulipwa riba ya asilimia 1.4.
Lakini Benki ya Stanbic, tawi la Tanzania iliongeza asilimia moja na hivyo kufanya serikali kutakiwa kulipa riba ya asilimia 2.4.

Post a Comment

 
Top