0


RAIS John Magufuli ametengua uteuzi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Juliet Kairuki kwa sababu mbalimbali, ikiwemo kutochukua mshahara wake tangu alipoteuliwa mwaka 2013.
 
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Profesa Adolf Mkenda, Dk Magufuli ametengua uteuzi huo rasmi kuanzia Aprili 24, mwaka huu. Profesa Mkenda alisema pamoja na mambo

mengine, hatua hiyo imechukuliwa na Dk Magufuli baada ya kupata taarifa kuwa mkurugenzi huyo alikuwa hachukui mshahara wa serikali tangu alipoajiriwa, jambo lililozua maswali.

Aidha, kwa mujibu wa Profesa Mkenda, endapo Kairuki atakuwa tayari kuendelea kufanya kazi na Serikali ya Awamu ya Tano, atapangiwa kazi nyingine. Alisema kutokana na hatua hiyo, tayari mchakato wa kumpata Mkurugenzi mpya umeanza mara moja.

“Wakati mchakato huo ukiendelea kwa sasa Clifford Tandali atakaimu nafasi ya Mkurugenzi Mtendaji wa kituo hicho,” alisisitiza Katibu Mkuu huyo. Kairuki anakuwa Mkurugenzi wa pili wa mashirika ya umma kutenguliwa uteuzi wake baada ya Rais Magufuli juzi kutengua uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dk Ally Simba.

Kairuki ni mtaalamu wa Sheria na masuala ya ubia kati ya Serikali na wawekezaji, na aliteuliwa kushika wadhifa huo Aprili 12, 2013 na Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete kutoka katika Chama cha Mabenki Afrika Kusini akiwa ni Meneja Mkuu wa Idara ya Benki na Huduma za Fedha.

Post a Comment

 
Top