0
Pele 
NYOTA wa zamani wa soka nchini Brazil, Edson do Nascimento (Pele), ameishtaki kampuni ya kutengeneza bidhaa za kielektroniki ya Samsung kwa kutumia mfano wa sura yake katika matangazo ya kibiashara bila idhini.

Pele ameitaka kampuni hiyo ya Korea Kusini imlipe dola za Kimarekani milioni 30, kutokana na kitendo hicho.

Mchezaji huyo wa zamani, amedai kwamba Samsung imekuwa ikitumia mfano wake katika tangazo la runinga aina ya Ultra High-Definition, katika jarida la New York Times bila idhini yake.

Mbrazil huyo mwenye umri wa miaka 75, aliwasilisha kesi hiyo katika mahakama ya Chicago nchini Marekani.

Pele anatambulika kama baba wa kizazi kipya cha soka, anafahamika duniani kote kwa ustadi wake wa kucheza mpira. Aliiongoza timu ya Brazil iliyotwaa kombe la dunia la mwaka 1958 na 1970.

Umaarufu wake haukuishia tu katika ushindi wa kombe la dunia, anakumbukwa kwa kuisaidia klabu yake ya Santos kutwaa ubingwa wa Copa Libertadores mara mbili, mbali na kunyakua kombe la Intercontinental.

Post a Comment

 
Top