RAIS Dk. John Magufuli, ameendeleza dhana yake ya kutumbua majipu viongozi wanaodaiwa kufanya ubadhilifu wa mali za umma kwa kumsimamisha kazi Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Wilson Kabwe akiwa kwenye daraja la Kigamboni.
Rais Magufuli alitoa uamuzi huo jana, wakati wa hafla ya ufunguzi wa Daraja la Kigamboni, baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kulalamikia utendaji mbovu wa Kabwe.
Makonda alisema utendaji wake huo umelisababishia Jiji la Dar es Salaam kupata hasara ya Sh bilioni 3 tangu mwaka 2009 hadi sasa.
Miongoni mwa mambo ambayo Makonda aliyalalamikia kwa kiongozi huyo mbele ya Rais Magufuli, ni ulanguzi wa kodi za pango za vyumba vya ofisi katika Stendi Kuu ya Mabasi ya Ubungo pamoja na kuongeza mkataba wa maegesho ya magari kinyume na utaratibu.
Makonda alitoa dukuduku lake hilo mbele ya Rais Magufuli baada ya mshereheshaji wa shughuli hiyo, kumpatia nafasi ya kukaribisha wageni kwa kuwa yeye ndiye mwenyeji wa mkoa huo.
Hata hivyo, wakati akiendelea na hotuba yake, Rais Magufuli alimwita tena ili amfafanulie juu ya sakata hilo ambalo alieleza kuwa lilifanywa na Kabwe pamoja na kaimu wake.
“Kuna jambo Mkuu wa Mkoa (Makonda) amelizungumza hapa, nataka aje atufafanulie zaidi nini hasa kilichotokea… hebu njoo,” Rais Magufuli alimwita Makonda.
Akifafanua sakata hilo, Makonda alisema kupitia kamati aliyoiunda, amebaini kuwapo mikataba tata ambayo Kabwe aliisaini na kusababisha Jiji kupata hasara hiyo.
“Kabwe alisaini mkataba mwaka 2015 tarehe 30 kwa kutumia ‘by law’ ya mwaka 2009 ambayo inaelekeza kila gari linaloingia Ubungo litatozwa Sh 8,000. Huyo huyo tarehe 31, 2015 akasaini tena mkataba mwingine kwa kutumia ‘by law’ ya mwaka 2004 ambayo inaelekeza kila gari litatozwa Sh 4,000.
“Matokeo yake mkandarasi ana mkataba mwingine wa ‘by law’ ya mwaka 2009 na Jiji lina mkataba wa ‘by law’ ya mwaka 2004 ambayo imekufa, hivyo kwa kukusanya Sh 4,000 kwa magari 300
yanayoingia Ubungo kila mwezi, tumekuwa tukipoteza Sh milioni 42 ambayo ukipiga hesabu kutoka mwaka 2009 hadi 2016, tumepoteza Sh bilioni 3,” alisema Makonda.
Alisema kwa upande wa maegesho ya magari, mkataba ulimalizika tangu mwaka jana na walitakiwa kutangaza zabuni, lakini hata hivyo, Kabwe na wasaidizi wake, walimwandikia barua aliyekuwa akisimamia maegesho hayo wakimtaka aendelee, kwa kile walichodai mchakato unaendelea.
“Walimwandikia barua ili aendelee na zabuni, awali walimwongezea miezi sita na baadae miezi minne, jumla walimpa miezi kumi nje ya utaratibu wa utangazaji wa tenda, na kila siku ‘parking’ zinaongezeka,” alisema Makonda.
Alisema kwa upande wa kodi za pango, ingawa kwa kawaida chumba kimoja cha ofisi Ubungo hutoza Sh 100,000, wamekuwa wakichukua pango hadi Sh milioni moja.
“Na watu wamekuwa wakitoa…hii ni rushwa na Kabwe ndiye amekuwa ‘signatory’ katika mikataba yote hii,” alisema Makonda.
MAGUFULI
Baada ya Makonda kutoa ufafanuzi wake huo, Rais Magufuli aliwauliza wananchi; “mnataka nimfanyeje huyu” na wao wakamjibu “tumbua”.
“Kwa kuwa Mkuu wa Mkoa umezungumza na niliapa kuisimamia sheria, viongozi hawa wanaofaidi jasho la masikini hawana nafasi. Hivyo namsimamisha kazi pamoja na kaimu wake… Watanzania wameteseka mno, sitakuwa na simile, pakitokea jipu sisubiri maana litaota usaha,” alisema.
Alisema viongozi wanaotaka kufanya kazi naye wajipange kuondoa mabaya katika uongozi wao, kwani wananchi wamechoka.
“Wananchi wamelia hadi machozi hayatoki, ni wakati wao sasa wa kufurahi na wale (viongozi mafisadi) walie, Kabwe akalie kule, naagiza achunguzwe, wa ‘kim-clear’ sitakuwa na tatizo, lazima kwanza achunguzwe.
“Wananchi mzidi kutuombea, na Makonda safi sana Mungu akubariki na uendelee kusimamia hivyo hivyo. Kupanga ni kuchagua na sisi tumechagua hivyo,” alisema Rais Magufuli.
Post a Comment