Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemtumia salamu za
rambirambi Waziri Mkuu wa Japan Mheshimiwa Shinzo Abe kufuatia vifo vya
watu zaidi ya 40 vilivyosababishwa na tetemeko la ardhi lililokikumba
kisiwa cha Kyushu
kilichopo kusini magharibi mwa nchi hiyo.Tetemeko hilo la ardhi limetokea Alhamisi iliyopita tarehe 14 Aprili, 2016 na kurudia tena siku ya Jumamosi tarehe 16 Aprili, 2016 ambapo limesababisha maporomoko makubwa ya udongo yaliyoharibu na kufunika makazi ya watu na miundombinu ya
usafirishaji na mawasiliano.
Katika salamu hizo zilizopitia kwa Balozi wa Japan nchini Tanzania Mheshimiwa Masaharu Yoshida, Rais Magufuli ameelezea kushtushwa na idadi kubwa ya watuwaliopoteza maisha katika ajali hiyo mbaya na amempa pole nyingi Waziri Mkuu wa Japan Mheshimiwa Shinzo Abe.
Aidha, Dkt. Magufuli amewapa pole wote waliojeruhiwa wakati wa maporomoko ya udongo, na amewaombea wapone haraka ili waweze kuungana na wananchi wengine wa Japan katika shughuli za kila siku za ujenzi wa Taifa lao.
Pia amevitakia kila la heri vikosi vya uokozi vinavyoendelea na kazi hiyo katika maeneo yote yaliyoathirika.
Post a Comment